SHU! Wakati Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi ikikutana
leo mjini Dodoma kupitia na mwishowe kukata majina ya wagombea
wanaowania kuteuliwa kwa nafasi ya Urais katika uchaguzi wa Oktoba mwaka
huu, presha ya muigizaji Jacob Stephen ‘JB’ imepanda, kwa hofu ya
kutokea tafrani miongoni mwa wanachama wa chama hicho.Muigizaji maarufu wa Bongo movie , Jacob Stephen ‘JB’ .
Akizungumza na gazeti hili juzi, JB ambaye ni kada wa chama tawala,
alisema tofauti na miaka ya nyuma alipokuwa akitambua wazi nani
atachukua nafasi hiyo, safari hii hali ni ngumu na kama CCM haitakuwa
makini, ipo hatari ya kutokea mgawanyiko mkubwa utakaosababishwa na
kukatwa kwa baadhi ya wagombea.
“Wakati Benjamin Mkapa akiwa madarakani, nilifahamu kwamba
atakayefuata ni JK (Jakaya Kikwete), lakini hali ya mwaka huu ni tofauti
kwa sababu haujui nani atafuata. Kwa sababu hiyo ipo haja, tena ya
makusudi kabisa kuhakikisha umakini wa hali ya juu unachukuliwa katika
kila hatua, vinginevyo inaweza kuleta matatizo makubwa,” alisema
muigizaji huyo mkongwe akiuzungumzia mchakato huo.
Kamati Kuu (CC-CCM) itaanza kikao chake cha kuchuja majina ya
wagombea hao wapatao 37 waliorejesha fomu, ili kupata majina matano
yatakayopelekwa mbele ya Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)
inayotarajiwa kukutana kesho, ambayo nayo itawakata wawili kati yao ili
watakaobaki waende kupigiwa kura kwenye Mkutano Mkuu utakaofanyika kwa
siku mbili za Jumamosi na Jumapili hii.
0 Comments