Makonda apewa siku saba kesi ya Guninita.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imetoa siku saba kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paulo Makonda, kuwasilisha utetezi wake dhidi ya kesi ya madai iliyofunguliwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida, Mgana Msindai na Mwenyekiti CCM mkoa Dar es Salaam, John Guninita.
 
Kesi hiyo namba 68 ya 2015, Makonda alitakiwa  kuwasilisha utetezi wake mahakamani jana, lakini wakili kupitia wakili wake, Lusiu Peter, ameomba Mahakama kumuongezea muda.
 
Hakimu Mkazi Mkuu, Hellen Riwa amekubali ombi la utetezi na ametoa siku saba kwa Makonda kuwasilisha uetetezi wake hadi  Aprili 23, mwaka huu.
 
Hakimu Riwa alisema kesi hiyo itatajwa  Aprili 27,mwaka huu.
 
Katika kesi ya msingi, Msindai na Guninita wanaiomba mahakama hiyo kumuamuru Makonda awaombe msamaha na kumlipa kila mmoja Sh. milioni 100. 
 
Wanadai fidia hiyo  kutokana na maneno ya kuwadhalilisha yanayodaiwa kutolewa na Makonda kama Katibu Uhamasishaji na Chipukizi wa CCM katika mkutano wake na waandishi wa habari.
 
Msindai na Guninita kupitia wakili wao, Benjamini Mwakagamba, wanaiomba Mahakama  pamoja na mambo mengine itoe zuio  la kudumu kwa Makonda  asizungumze  tena maneno ya kashfa wala kuyasambaza kama alivyofanya awali.

Post a Comment

0 Comments