Agosti 12 nilipata wasaa wakutembelea hospitalini kidogo, kama ujuavyo
aendae hospitalini ni mgonjwa, basi, nilienda huko, kisa ili kuweza
kujua hali yangu ya kiafya. Maana mara ya mwisho kutembelea hospitalini
ni mwaka 1984 wakati wa sindano za ndui. Nilijongea KATIKA HOSPITALI
MOJA ILIYOPO JIJINI Dar es Salaam na kuweza kufuata taratibu zote.
Lakini kabla ya kuanza safari, huko nyumbani kwangu, mke wangu nayeye
alihitaji kwenda kwa tabibu kupata matibabu ya jino lake ambalo nalo
lilikuwa likimsumbua kwa muda mrefu. Kama ujuavyo msomaji wa makala
haya, dawa ya jino kung’oa! Kwa kuwa leo hii mzee wa kazi niliamua
kwenda hospitali nayeye mama watoto wivu ukamjia.
Tulifanya safari ya kuelekea huko, unajua tena siye wazee wa madogo
poromoka-pangu pakavu tia mchuzi, tulianza kwa kutembea mwendo wa dakika
20, tukapanda daladala kuelekea huko hosptalini na unajua tena lazima
uzunguke na gari angalau abiria kuweza kukaa kwenye kiti.
Utaratibu wa Bima ya Afya
Tukiwa nyumbani, kila mmoja alibeba kitambulisho chake cha BIMA YA AFYA
na kufuata utaratibu wa hospitali hiyo. Wajino akaenda kwa daktari wa
meno na mie wa mguu nikaenda kwa dakitari wangu.
Mwezangu akaenda kwa wa meno akapata maelekezo juu ya kuzibwa kwa jino
lake lililokuwa linamsumbua. Mwenzangu alimaliza mapema kupata huduma,
madaktari wana mambo kweli kweli, yaliyofanyika huko ndani mie sijui ila
nasema niliyosimuliwa tu. Kwa bahati nzuri nilikutwa sijaenda kumuona
tabibu kulikuwa na foleni ndefu sana. Mamaa alinikuta na kuniuliza
daktari wa ndani ni mwanamke au mwaname nikasema mie sijui.
Nikaingia kwa daktari na kukutana na tabibu mwanamke mrembo na daktari
huyu aliniuliza kilichokuwa kinanisibu na nikapewa maelekezo ya cha
kufanya ambapo niliambiwa nifanye vipimo na majibu nisiyachukue kwa siku
hiyo, basi kwa kuwa nilikuwa mgonjwa mtiifu na nilifuata utaratibu wa
daktari na kuelekea kwenye vipimo, mke wangu akiwa nyuma yangu
Basi nilifika nje ya mlango wa miale ya x na mhusika alianza kwa kuita
majina ya wanaoingia humo, lilitajwa jina la kwanza, hakuna aliyeitika,
la pili nalo vivyo hivyo na jina la tatu lilikuwa langu. Nikapewa
maelekezo niingie chumbani, mwanadada aliliita jina langu kwa kulikatiza
huku wagonjwa wengine wakidhani anayeitwa ni mwanamke. Kumbe ni
mwanamme na tena baba wa watoto kadhaa.
Kwa nyuma yangu ikasikika minong’ono ”Huyu dada vipi mbona
anamdhalilisha huyu baba kwanini kamuita Adela? Mke wangu akasema, jina
lake ni Adeladius, huyu nesi amekatisha tu.” Mambo ya Ngoswe mwachie
Ngoswe mwenyewe. Mie nikaingia ndani.
Sikuweza kusema neno kwa kukatishwa jina langu akisema mkeo umesema
wewe, kwa kuwa unapokuwa hospitali ni ulimwengu wa matabibu ukileta
mchezo shauri yako, nilikuwa baba au kijana mtiifu sana. Nilipoingia
ndani alikuja mama mmoja mrefu, akiuliza, wewe mbona unamuita mgonjwa
mwingine na kumsahau mgonjwa wangu? Yule dada mhusika aliyeniita kwa
kukosea jina langu akajibu kwa kunitazama mimi, eti kaka nimeita karibu
mara ngapi hakuna aliyekuja? Mie nikajibu mama uliita mara tatu.
Basi nikaelekezwa cha kufanya na kupanda katika kitanda kikubwa cha
chuma na kupigwa picha ya miale ya x na kuelekea hatua ya pili ya vipimo
vya damu. Lakini kumbuka nilijulishwa na tabibu wangu kuwa majibu
yatachukuliwa kesho saa saba mchana ili yaweze kufanyiwa tafsiri na
wahusika.
Kweli mumeo anakupenda?
Nilitoka na kuanza safari ya kurudi kwetu madogo poromoka;Tukiwa njiani kila mmoja wetu anamuuliza mwezake hali ya matibabu. Mamaa
akasema unajua nilipoenda kwa daktari nilitaka kwenda kung’oa jino
maana lilikuwa linanisumbua sasa daktari kaniuuliza yani mumeo
amekuruhusu kung’oa jino la mbele tena jino la kicheko, Kwelimumeo
anakupenda? Maana hilo jino likitolewa tambua kuwa muonekana wako
hautakuwa mzuri.
Lakini msomaji wa makala haya kupitia tovuti ya TBC mimi nilitoa ruhusa
kwa kuwa mke wangu kwani alikuwa akilalamikia maumivu ya jino hilo kama
nilivyokwambia hapo awali kuwa raha ya jino kung’oa
Basi tukafika nyumbani kwetu na kumbuka mie nilipewa maelekezo ya
kumuona daktari wa kike siku inayofuata na mke wangu alipewa maelekezo
ya kumuona daktari siku ya alhamisi. Kulipokucha niliamka mapema na
kupitia kazini kupewa kibali cha kuelekea kwa tabibu ili kuchukua vipimo
na kujua kipi kilikuwa kinanisumbua basi nilifika hospitali na kama
kawaida mambo ya foleni nikaandikisha na kufuata majibu ya vipimo
vyangu.
Ulimwengu wa Tekinolojia
Nikiwa hospitalini niligundua mengi hasa kuwa sasa ni ulimwengu wa
tekinolojia kila linalofanyika linawekwa kwenye mtandao sasa hivi
mafaili ya wagonjwa yanakuwa ya kimtandao na sio mafaili ya karatasi ya
zama zile, nilimfuta tabibu na kupewa majibu ya vipimo vyangu na kupewa
tiba huku daktari akitazama faili langu katika kompyuta yake.
Niliporudi nyumbani mamaa aliniuliza maswali mengi juu ya matibabu yangu
na kubwa ni kwanini tabibu alinipangia niende kesho yake. Basi
nilimwambia kuwa vipimo vyangu vilihitajika kufanyiwa tafsiri ndiyo
maana niliambiwa kurudi kesho yake na nimepewa matibabu na ninamshukuru
sana daktari huyo.
Yangu mie yalimalizika jana ila leo hii mke wangu anaenda kuziba jino
lake kwa daktari yuleyule aliyemuuliza mke wangu kama kweli nampenda.
Yeye ndiye ametoa ushauri wa jino la mke wangu kuzibwa badala ya
kung’olewa, lakini mie ninaamini katika kuheshimu taaluma yoyote ile.
Kwa upande wangu nilipata dawa nzuri za daktari yule mrembo, kama
unaleta wivu basi wewe hautaki kupona hospitalini, mie nataka kupona
kama ilivyo kwa mke wangu. Ninachojilaumu ni kimoja tu nilisahau kuomba
nambari ya simu ya daktari wangu angalau siku nyengine ningempigia simu
kumueleza hali yangu inavyoendelea. Msomaji wa makala haya je
nimechelewa kuiomba nambari ya simu ya tabibu huyu? Binafsi ninaamini
sijachelewa nitaenda kumuomba nambari yake ya simu daktari wangu
0 Comments