Kwa ufupi
Jambo linalochangia Yanga kuwa na wakati mgumu
katika mechi dhidi ya Simba ni kwamba wanakuwa katika presha kubwa ya
mchezo kuliko Simba.
Dar es Salaam.Vikao virefu, vitisho vya wazee pamoja na baadhi
ya viongozi wakiwatuhumu wachezaji sita kuhujumu timu hiyo vimetwaja
kuwa ni sababu ya Yanga kufungwa na Simba juzi kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Yanga ilifungwa na Simba bao 1-0 juzi, shukrani
kwa bao la Emmanuel Okwi alilolifunga kwa shuti la umbali wa mita 35 na
kuwazima mashabiki wa Yanga waliofurika uwanjani hapo wakiamini
watashinda mchezo huo.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema kwamba siku
mbili kabla ya mchezo wazee wa klabu hiyo walitua kambini usiku na
kuzungumza na wachezaji hadi usiku wa manane, huku wakiwachimba mikwara
iliyochangia kuwatisha baadhi ya wachezaji na kuwatoa mchezoni.
Chanzo hicho kilisema wazee hao waliwaambia
wachezaji wao kuwa wanasikia kuna baadhi wamehujumu mechi hiyo hivyo
wanatakiwa kuwa makini kwani wamechoshwa na mashabiki wao kufa kwa
presha uwanjani kutokana na matokeo mabaya wanayopata kutoka kwa Simba.
“Yaani wachezaji walipigwa mkwara kabla ya mchezo
ule na wazee wa klabu ambao walikwenda kuzungumza na wachezaji Ijumaa
usiku na walionekana kabisa wamepania kwani walionekana wanaongea kwa
jazba na wachezaji wengi waliingiwa na hofu,”kilisema chanzo chetu hicho
cha habari.
Wachezaji waliodaiwa kuhujumu timu hiyo kwa
kucheza chini ya kiwango ni pamoja na kipa Ali Mustapha ‘Barthez’, Simon
Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Danny Mrwanda pamoja na Kelvin
Yondani.
Hata hivyo, Mustapha’Barthez’ alikuwa kwenye
wakati mgumu zaidi akitakiwa kuwa makini golini na asifungwe mabao ya
kizembe kama alivyofanya kwenye mechi ya ligi msimu uliopita
iliyomalizika kwa sare ya 3- 3.
Barthez juzi alifungwa bao la umbali wa mita 35 na
Okwi, lililosababisha baadhi ya mashabiki kumtafuta kwa lengo la
kumpiga, lakini Polisi walimuokoa na kumuingiza kwenya basi la wachezaji
na kulisindikiza hadi lilipoondoka.
Baada ya kipenga cha mwisho cha mwamuzi Martin
Saanya, kipa huyo alimwaga machozi na aliendelea kulia hata alipoingia
katika vyumba vya kubadilishia nguo na hivyo kuwapa kazi wachezaji
wenzake kumbembeleza.
Wachambuzi wanena
Wachambuzi wa masuala ya soka nchini wamesema
kufungwa kwa Yanga kumechangiwa na kocha Hans Pluijm kwanza kuchezesha
nusu ya kikosi chake washambuliaji, pili kuwa na wachezaji wenye umri
mkubwa na tatu wachezaji kuathirika kisaikolojia.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti
jana, wachambuzi hao, Edo Kumwembe na Kenny Mwaisabula walisema,
wachezaji wenye umri mkubwa na kitendo cha kufungwa mara kwa mara na
Simba na mfumo wa timu uliotumiwa na Pluijm ndivyo vilizamisha jahazi la
Yanga huku kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ akikingiwa kifua kwa bao
alilofungwa.
0 Comments