Dar es Salaam. Nahodha wa Simba, Hassan Isihaka amesema kinachowasumbua sasa Yanga ni umri wa wachezaji wao.
Simba iliifunga Yanga bao 1- 0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Isihaka aliiambia Mwananchi kuwa kikosi cha Simba
kina wachezaji wengi vijana kuliko Yanga ndio maana wanaonyesha kiwango
bora uwanjani kuliko wapinzani wao.
Alisema kila mmoja aliona jinsi Simba ilivyotawala
mchezo kutokana na kuwa na damu changa ambazo zilisababisha wakacheza
soka la kasi na pasi nyingi.
“Tunafurahi na watu lazima wajue mpira ni magoli
na burudani, hivyo tunaamini tumewaburudisha mashabiki wetu kwa soka
safi tulilocheza, kila mtu aliona tulikuwa bora kuliko wapinzani wetu
Yanga.
“Kinachotusaidia sisi tukawa bora uwanjani ni aina
ya wachezaji tuliopo katika timu yetu, wengi ni vijana na ndio kwanza
timu inajengwa hivi sasa kupitia damu changa tofauti na Yanga wachezaji
wao wengi na wamekaa na timu muda mrefu, hivyo watasubiri sana kwetu,”
alisema Isihaka.
Hata hivyo Isihaka aliwataka wenzake kuendelea
kupambana katika michezo mingine ijayo na ushindi huo usiwafanye
wakaridhika mapema bali uwe chachu ya kufanya vizuri kwa mechi nyingine.
“Bado tuna safari ndefu, sawa tumepata ushindi
lakini hatupaswi kuridhika, tunahitaji kupambana zaidi, tunatakiwa
kushinda michezo mingine yote iliyobaki, kwani ligi ya msimu huu ni
ngumu sana.
“Ushindi dhidi ya Yanga uwe chachu ya kufanya
vizuri katika mechi zinazokuja, ni ushindi ambao umerudisha morali ya
timu na umetupa furaha pia hivyo tunatakiwa kujituma , kupambana na
kumaliza tukiwa katika nafasi mbili za juu kwani hao waliotangulia
wanaweza kupoteza hivyo hatupaswi kukata tamaa,” alisema Isihaka.
Kwa ufupi
Simba iliifunga Yanga bao 1- 0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
0 Comments