SASA ni wazi kuwa waziri mkuu wa zamani, Edward Ngoyai Lowassa ndiye
atakuwa rais wa awamu ya tano Tanzania mwaka 2015, kutokana na ukweli
kwamba kambi zinazosigana ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM),
zinaonekana kupwaya huku yake ikiwa na watu wenye nguvu kisiasa na
kiuchumi, Risasi Jumamosi linakuwa la kwanza kusema.
Katika vuguvugu la nani awe rais mwaka 2015, uchunguzi wa gazeti hili
ulionesha kuwa tangu uchaguzi ndani ya chama hicho mwaka jana, Lowassa
anaonekana kupata mafanikio zaidi kisiasa, ikilinganishwa na mahasimu
wake, Benard Membe na Samuel Sitta ambao wanatajwa kutaka kuwania urais
baada ya Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kumaliza muda wake.
Kama ilivyo kwa Lowassa, Sitta ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki na Membe mwenye kofia ya Uwaziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, nao wamekuwa wakidaiwa kuwa na makundi katika
harakati za kuusaka urais, japokuwa wenyewe hawajathibitisha.
Uchunguzi huo umeonesha kuwa Lowassa ana mtandao wenye nguvu kisiasa
na wachunguzi wa mambo wanasema hata kama vikao vya juu vitamkata jina,
kundi lake likiamua nani awe rais uwezekano wa mtu huyo kupita ni
mkubwa.
Katika uchaguzi wa chama katika mikoa, wafuasi wengi wa Lowassa
walipeta ukilinganisha na makundi mengine yanayotajwa katika
kinyang’anyiro cha urais.
Baadhi ya wasomi nchini, walitofautiana kimtazamo kuhusu chaguzi hizo
ndani ya CCM. Mhadhiri maarufu wa UDSM, Dk. Benson Bana alisema CCM
katika chaguzi hizo imeonesha kwamba hakuna kiongozi yeyote mwenye hati
miliki ya chama hicho kwani mtu yeyote anaweza kuingia na kuondoka
kwenye chama hicho.
Naye Kisena Mabuba ambaye ni Mhadhiri katika Chuo cha Kumbukumbu ya
Mwalimu Nyerere alisema: “Tofauti na matarajio ya wengi kuwa CCM
ingemeguka, mimi ninachokiona hapa kundi lililobaki na nguvu ni lile la
mwenyekiti mwenyewe. Kundi moja limefutwa kabisa na mengine yameshindwa
kupata nguvu za kutosha.”
0 Comments